Shughuli mbalimbali za kijamii katikati ya jiji la Mwanza zimesimama kwa zaidi ya saa moja,wakati mamia ya wafuasi wa chama cha demokrasia na maendeleo ( CHADEMA ) walipokuwa wakitoka mahakama kuu kanda ya Mwanza kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi jimbo la Nyamagana iliyofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Ezekiel Wenje.
Wafuasi hao wa CHADEMA walifunga mitaa yote ya jiji la Mwanza,
majira ya saa sita mchana wakati wakitoka Mahakamani kusikiliza kesi ya
uchaguzi namba 3 ya Mwaka 2016, iliyofunguliwa na Ezekiel Wenje dhidi ya
mbunge wa sasa wa jimbo la Nyamagana Mh.Stanslaus Mabula hatua
iliyosababisha baadhi ya maduka kufungwa na usafiri wa daladala kusimama
kwa muda kwa hofu ya kuibuka vurugu.
ITV imeshuhudia Defender za polisi zikiwa na askari wa kikosi cha
kutuliza ghasia ( FFU ),wenye silaha za moto na mabomu ya machozi
zikifanya doria katika mitaa ya katikati ya jiji pamoja na viunga vya
mahakama kuu, ambako tangu asubuhi mamia ya wafuasi wa CHADEMA
wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho taifa Mh. Freeman Mbowe
walikuwa wamepiga kambi kwa ajili ya kufuatilia kesi hiyo inayosikilizwa
na jaji kakusulo sambo.
Wafuasi hao wa CHADEMA ambao walitoka Mahakamani hapo wakikimbia
huku wakiimba na kushangilia kuelekea Hoteli ya Gold Crest,baadhi yao
walijikuta wakiwa mikononi mwa Polisi na wengine kupata Mkong’oto na
kuswekwa rumande kwa kushindwa kutii amri halali ya polisi iliyowataka
kuwa watulivu,jambo ambalo limelalamikiwa na baadhi ya wafuasi hao
katika mahojiano na ITV.
Katika hatua nyingine jaji wa mahakama ya rufaa Mh.Rosemary Ibrahim
ametupilia mbali kwa gharama maombi ya kesi ya kupinga matokeo ya
uchaguzi mkuu wa oktoba 25 Mwaka jana, yaliyokatiwa rufaa na wapiga kura
wanne wa jimbo la bunda mjini dhidi ya mbunge wa jimbo hilo Mh. Esther
Bulaya,kufuatia makosa ya kisheria yaliyojitokeza kwenye kiapo
kilichoapwa na mtu mwingine na kuthibitishwa na mtu mwingine.
Jaji Ibrahimu amesema Mahakama hiyo imeamua kutoa uamuzi huo
kulingana na sheria zinavyoelekeza baada ya wakili wa wapeleka maombi
Costantine Mutalemwa na Denis Kahangwa kukiri kuwapo kwa kosa hilo na
kutoa mifano ya kesi zilizowahi kuamriwa na mahakama nyingine kwa
kuonyesha hazikuwa na makosa kama hayo bali aliyeapa kiapo hicho ndiye
aliyethibitisha ila kulikuwa na makosa madogomadogo yaliyokubalika
kufanyiwa marekebisho tofauti na hilo.
Taarifa >>>>>ITV
Kesi ya Wenje Kusimamisha Shughuli Mwanza.
4/
5
Oleh
kwetutz24